MWANAMKE mmoja aliyefahamika kwa jina la Subira Malefya (53), mkazi wa
kijiji cha Ipinda, kata ya Ipinda, wilayani Kyela, amelazwa katika hospitali ya
wilaya Kyela baada ya kuunguzwa vibaya mwili mzima na mumewe usiku wa kuamukia
juzi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Katibu, tarafa ya Ntebela,
Cuthberty Mwalukama, akiwa amelala mwanamke huyo alimwagiwa mafuta ya taa mwili
mzima kabla ya kumwasha moto kwa kiberiti ikiwa ni usiku wa saa 4:00.
Alisema baada ya mume huyo kufika nyumbani akiwa amelewa wakati huo mkewe
akiwa amelala na wajukuu zake, ndipo akaenda dukani kununua mafuta ya taa kiasi
cha lita moja na nusu na kiberiti, kisha kummwagia mkewe na kumtia kiberiti.
Katibu tarafa huyo alifafanua kuwa mume wa mwanamke huyo ambaye ni mwalimu
mstaafu, Boniphace Mwakinyuke (64), yeye na mkewe walikuwa pamoja klabuni siku
hiyo, lakini mke aliwahi kuondoka, kitendo ambacho kinadhaniwa kumkera mumewe.
Alisema baada ya tukio hilo , wananchi wa eneo
hilo walitoa
msaada wa kumkimbiza hospitalini mwanamke huyo katika kituo cha afya Ipinda
akiwa mahututi na baada ya kupatiwa matibabu ya awali, walimkimbizia hospitali
ya wilaya kwa matibabu zaidi.
Aliongeza kuwa mbali ya wasamaria hao kumsaidia mwanamke huyo, pia
walimkamata mtuhumiwa huyo na kumfikisha katika kituo kidogo cha polisi cha
Ipinda kabla ya kupelekwa kituo kikuu cha polisi wilayani Kyela, anakoshikiliwa
kabla ya kufikishwa mahakamani kwa taratibu zaidi za kisheria.
Naye mganga mkuu wa wilaya Kyela, Festo Ndungange, amekiri kumpokea mgonjwa
huyo ambaye amelazwa kwenye wodi namba 3 akisema wanajitahidi kumhudumia
kumpunguzia maumivu anayoyapata.
Chanzo cha habari na gazeti
la Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment