HATIMAYE
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali pingamizi
lilowasilishwa mbele yake na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, lililokuwa likiomba mahakama
hiyo ifute kesi ya madai iliyofunguliwa na Rose Kamili Slaa aliyeomba
imzuie mumewe Dk. Slaa asifunge ndoa na mchumba wake, Josephine
Mushumbusi.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Laurence Kaduri ambaye alisema
baada ya kupitia kwa kina pingamizi lilowasilishwa na Dk. Slaa na
majibu yaliyojibiwa na mlalamikaji Rose anayetetewa na wakili wa
kujitegemea Joseph Thadayo, ameona hoja za kutaka mahakama iifute kesi
ya msingi iliyofunguliwa na Rose ni dhahifu na hivyo amezitupilia mbali.
Jaji Kaduli alisema Dk. Slaa alikosea kudai kuwa Rose hakuwa na
haki ya kufungua kesi hiyo ya kumzuia asifunge ndoa na mchumba wake,
Josephine, kwa sababu hawakuwahi kufunga ndoa ila kulikuwa na dhana ya
ndoa.
“Mahakama hii inaitupilia mbali tena kwa gharama pingamizi hilo la
Dk. Slaa linalosema kuwa Rose hakuwa na haki ya kupinga ndoa yake kwa
sababu hakuwa mke wake na wala hawajawahi kufunga ndoa kwa sababu
sheria ya ndoa inasema mtu ambaye umeishawahi kuishi kama mke na mume
kwa zaidi ya miaka miwili, inawahesabu kama ni wana ndoa.
“Hivyo mahakama hii inasema Rose ana haki ya kufungua kesi ya
kuzuia ndoa ya wadaiwa, yaani Slaa na Josephine na natupilia mbali
pingamizi la Slaa na kwamba kesi ya msingi itakuja kutajwa mahakamani
hapa Novemba 6 mwaka huu,” alisema Jaji Kaduri.
Kesi hiyo ya madai ya ndoa ilifunguliwa mahakamani hapo na Rose
dhidi ya Dk. Slaa na Josephine kwa mara ya kwanza mapema Julai mwaka
huu, akiiomba mahakama isikubali shauri hilo lipelekwe kwenye Bodi ya
Maridhiano ya Masuala ya Ndoa kwa ajili ya kupatanishwa.
Dai la pili, Rose anaiomba mahakama itangaze yeye na Dk. Slaa bado
ni wanandoa, na dai la tatu anaiomba mahakama itamke kuwa ndoa baina
yake na Dk. Slaa bado halali kisheria na kwamba ndoa nyingine
itakayofungwa kinyume na sasa itakuwa ni batili. Katika dai lake la
nne, mlalamikaji ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), anadai
mdaiwa wa pili (Josephine) alimshawishi mumewe kuivuruga ndoa yake.
Pia nia ya wadaiwa hao wawili ya kutaka kufunga ndoa waliyopanga
ifungwe Julai 21 mwaka huu katika eneo lolote lile, ndoa hiyo ihesabike
kuwa ni batili.
Aidha, anaiomba mahakama iwaamuru wadaiwa wamlipe fidia ya shilingi
milioni 50 kama gharama za matunzo ya watoto wawili ambao ni Emiliana
Slaa na Linus Slaa aliyezaliwa mwaka 1987 ambao amekuwa akiwahudumia
tangu mwaka 2009 baada ya mume wake kumkimbia.
Pia anaiomba mahakama imwamuru mdaiwa wa pili (Josephine) amlipe
fidia ya sh mil. 500 kwa sababu alimsababishia usumbufu mkubwa na
kumharibia ndoa yake, na kuongeza kwa kuiomba mahakama hiyo impatie
nafuu nyingine ambazo itaona inafaa.
Happyness Katabazi-Dar-se-salaam
0 comments:
Post a Comment