MAKUNDI
ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), yanaonekana kumwelemea Mwenyekiti
wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, na sasa ameamua kutumia mkutano
mkuu wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT), kukemea vitendo vya
kudhalilishana na makundi wakati na baada ya uchaguzi.
Rais Kikwete pia alionya juu ya vitendo vya rushwa vinavyozidi
kushamiri ndani ya chama hicho akisema kuwa visipochukuliwa hatua
mapema, kuna hatari ya kukifikisha chama katika hatua mbaya.
Akifunga mkutano huo wa nane wa uchaguzi UWT, Rais aliwataka kufanya jitihada za kupunguza mgawanyiko uliotokea
baada ya uchaguzi wao uliomalizika juzi.
Alisema imekuwa ni hulka sasa hasa baada ya kumalizika uchaguzi kwa
wanachama kuendeleza na kuwekeana uhasama kama uliokuwepo wakati wa
kampeni na wengine kuwaadhibu ambao hawakuwachagua hali ambayo ni mbaya
sana kwa mustakabali wa chama.
“Ambaye hakukuchagua usimbague kwani hakushinda na sasa wewe ndiye
kiongozi, hivyo una kila sababu ya kumpa ushirikiano ili aweze
kutekeleza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuitumikia jumuiya yake
kwa ukamilifu.
“Itakuwa ni aibu sana na ajabu, pia utakuwa hujatenda haki kwa
kumbagua ambaye hakukuchagua; natolea mfano kwangu katika uchaguzi
uliopita, Prof. Mark Mwandosya hakushinda, lakini kwenye serikali yangu
nilimuweka licha ya kuwa nilifanyiwa mambo ya ajabu sana ambayo ni
vigumu kuyavumilia lakini kwa mwanasiasa, lazima uwe mkomavu,”
alisisitiza.
Rais Kikwete aliwaasa wagombea wa nafasi mbalimbali wa UWT
walioshindwa kutoweka visasi na walioshinda kutowapiga vijembe
walioshindwa kwani kazi iliyo mbele ni kubwa kutokana na CCM hivi sasa
kukabiliwa na hali ngumu ya ushindani wa kisiasa.
“Kweli tusipokemea vitendo hivi na kuviacha vikiendelea,
tutakipeleka chama mahali pabaya, ninasikitika sana kusikia hata
wanawake sasa wanajihusisha na utoaji rushwa ili kununua nafasi za
uongozi kitu ambacho ni hatari sana,” alisema Kikwete.
Alifafanua kuwa chama kinakoelekea si kuzuri ni lazima zifanyike jitihada za mabadiliko.
Aliwapongeza wajumbe kwa kukamilisha uchaguzi wa viongozi
watakaoongoza jumuia hiyo kwa muda wa miaka mitano na hata
waliojitokeza kugombea kwani kuvunjika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi.
Rais Kikwete aliongeza kuwa madhumuni ya CCM yaliyotamkwa katika
katiba ni kushinda katika uchaguzi wa serikali kuu na mitaa Tanzania
Bara na Zanzibar ili kuunda serikali kuu na serikali za mitaa.
Alisema ushindi wa CCM unapatikana kwa kukubaliwa na kuungwa mkono
na wananchi wengi zaidi watakaojitokeza kupiga kura, hivyo kazi kubwa
ambayo inatakiwa kufanywa na jumuiya za chama zilizoundwa ni
kufanikisha hilo.
Kikwete alifafanua kuwa demokrasia ya uchaguzi ina athari zake
kwani baada ya hapo kuna kazi kubwa ya kujenga umoja na mshikamano ili
kuziba nyufa na mipasuko iliyotokea wakati wa uchaguzi.
Alisema kuwa huwezi kumchukia mwenzako kwa vile ameomba nafasi
unayoitaka wewe, kwamba nafasi hiyo ni haki ya kila mwanachama, hivyo
hakuna haja ya kuchukiana.
Rais Kikwete alifafanua kuwa uchaguzi una mifarakano mingi lakini
kiongozi akishapatikana ni lazima aungwe mkono na kwamba wenye
kuonyesha mfano ni wale walioshinda kwa kutowabeza walioshindwa.
Awali, Mwenyekiti wa UWT, Sophia Simba, alisema kuwa wamefanya
mengi ikiwemo kuongeza idadi ya wanachama na wamejipanga kuhakikisha
wanaleta ushindi katika uchaguzi mkuu wa 2015.
chanzo cha habari-Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment