UCHAGUZI mdogo wa udiwani katika kata ya
Darajambili Mkoani Arusha leo umeingia dosari baada ya risasi kurindima hewani
mfulululizo asubuhi ya leo karibu na maeneo ya kupigia kura hali iliyozua taharuki kwa wakazi wa kata hiyo waliokuwa
wamejitokeza katika vituo vya kupigia kura.
Risasi hizo zinadaiwa kupigwa na mbunge wa jimbo la
Arumeru Mashariki,Joshua Nassari pamoja na mwenyekiti wa Umoja wa vijana wa
CCM(Uvccm) wilayani Arusha,Godfrey Mwalusamba mara baada ya kuibuka tafrani
baina ya wafuasi wa CCM na Chadema katika eneo la Shule ya sekondari ya Felix
Mrema.
Katika vurugu hizo dereva wa aliyekuwa Mbunge wa
Arusha Mjini Haleluya Natai pamoja na wafuasi wa Chadema zaidi ya 15
walikamatwa na jeshi la polisi huku Nasari na aliyekua mbunge wa jimbo la
Arusha mjini Godbles Lema wakitokomea kusikojulikana lakini kisha baadaye
walionekana katika viunga vya kupigia kura.
Hatahivyo,katika hali isiyo ya kawaida naye mgombea wa
Chadema katika kata hiyo,Prosper Msofe alionekana akirandaranda katika vituo
vya kupigia kura huku akiwa na silaha yake aina ya bastola kiunoni hali ambayo
ilizua mshangao kwa wapiga kura wa kata hiyo.
Katika vurugu hizo inadaiwa kuwa Nasari aliyekuwa
akiongozana na lema wakiwa katika gari mojawapo walivamia ngome ya CCM iliyopo
karibu na ofisi za chama hicho kata ya daraja mbili hali ambayo ilipelekea
wafuasi wa CCM kuwavamia lakini Nasari alijiami na kisha kufyatua risasi tatu
hewani.
Hatahivyo,kada wa CCM ,Kabwelwa Mturuka alijeruhiwa
mkononi kwa kukatwa na panga na watu wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa Chadema
wakati wa majibishano karibu na kituo cha kupigia kura.
Katika vurugu hizo mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya
Arusha Martin Munis naye aliporwa simu yake ya mkononi na fedha ambapo
alitoa taarifa katika jeshi la polisi na kupewa AR/RB/13624/2012 ya shambulio
la kudhuru mwili dhidi ya Nasari na Lema.
Wakati huohuo,wafuasi wa Chadema waliokuwa mita chache
karibu na kituo cha kupigia kura cha sekondari ya Felix Mrema baada ya zoezi la uchaguzi kwisha, wakati wakisubiri matokeo, walivamia ofisi
za CCM zilizokuwa karibu na kituo hicho na kisha kujaribu kung”oa bendera ya
chama hicho lakini jitihada hizo zilizimwa na wafuasi wa CCM baada ya kumshusha
kabla hajaikaribia bendera hiyo.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Arusha,Liberatus
Sabas alipoulizwa juu ya matukio hayo alisema kwamba ni mapema sana
kuzizungumzia lakini alikiri kushikiliwa kwa baadhi ya wafuasi wa CCM na
Chadema ambao walihusika na vurugu katika uchaguzi huo.
Kwa upande wake,Nasari alipoulizwa juu ya hatua yake
ya kurusha risasi hewani alipinga vikali lakini alipotafutwa Mwalusamba alikiri
kurusha risasi hizo hewani huku akidai kwamba alifyatua kwa lengo la kujihami.
Aidha saa nne usiku matokeo yamekemilika na kutangazwa na Modest Lupogo kwa niaba ya kaimu mkurugenzi wa jiji la Arusha Omary Mkombole ambapo alisema kuwa idadi ya watu walioandikishwa kupiga kura ni 16295 lakini waliojitokeza kupiga kura ni 3770 tu.
Akutangaza mshindi (diwani mpya wa kata ya daraja mbili)Lupogo alisema kuwa Prosper Msofe aliibuka kidedea kwa kura 2193 kupitia Chadema, akifuatiwa na mpinzani wake Philip Mushi Philip kupitia CCM aliyepata kura 1324, huku CUF ikipata kura 162, TLP wakipata kura 42, na NSSR kuambulia kura 22
Wakati huo huo katika kata ya Bangata iliyoko wilayani Arumeru mkoani Arusha akitangaza matokeo hayo mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Arusha Halipha Idda alisema kuwa Olais Peter kupitia CCM ameibuka kidedea kwa kura 1177 na kuwaacha wapinzani wake Erick Samson Mollel kupitia Chadema kwa kura 881 huku Samweli Saimon Ndosi kupiti TLP akiambulia kura 3
0 comments:
Post a Comment