.

.
Tuesday, October 23, 2012

11:30 AM

WENYEVITI wa vitongoji na vijiji wilayani Ukerewe, Mwanza wanaodai posho ya kusimamia Sensa ya Watu na Makazi, wamepitisha azimio la kumshitaki mahakamani mkuu wa wilaya hiyo.


Wenyeviti hao wa vitongoji na vijiji wapatao 256 walipitisha azimio hilo jana katika kikao chao kilichofanyika mjini hapa.


Viongozi hao walifikia uamuzi huo baada ya kutoridhishwa na majibu yanayotolewa na Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Mariam Mseleche na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Joseph Mkundi, ambao nao walishiriki kikao hicho.


Mwenyekiti wa Umoja wa Wenyeviti wa Vitongoji na Vijiji wa wilaya hiyo, Hussein Hassan, alisema mbali ya azimio hilo pia wamekubaliana kususia shughuli zote za maendeleo na kuongeza kuwa hivi sasa wanawasiliana na wanasheria, ili suala hilo walifikishe mahakamani kwa utatauzi wa kisheria.


Katika madai yao, kila mwenyekiti wa kitongoji anadai posho ya sh 140,000 pamoja na posho ya madaraka ya kila mwezi ambayo hawajalipwa tangu Septemba mwaka jana mpaka sasa.


Katika hatua nyingine viongozi hao wa vitongoji na vijiji wametaka posho ya madaraka kwa wenyeviti wa vitongoji iongezwe kutoka sh 5,000 ya sasa hadi sh 35,000 kwa mwezi huku wenyeviti wa vijiji wakitaka iongezwe kutoka sh 10,000 hadi 50,000.


Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Mariam Mseleche, akizungumzia madai hayo alisema yapo nje ya uwezo wake na kuaidi kuyafikisha katika mamlaka husika.


Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Joseph Mkundi, ameahidi kufuatilia na kupata ukweli wa madai ya kutolipwa posho ya madaraka na kulipatia ufumbuzi.
chanzo cha habari:Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment