BAADHI ya wakazi wa Kijiji cha Igombe,
Kata ya Bugogwa katika Manispaa ya Ilemela, jijini Mwanza, wanajisaidia
kandokando mwa Ziwa Victoria na kusababisha uchafuzi wa mazingira.
Hali hiyo imebainika hivi karibuni wakati wa ziara ya waandishi wa
habari za mazingira walipotembelea eneo la mwalo wa Igombe na kujionea
vinyesi vya binadamu vilivyotapakaa huku shughuli za kilimo zikiendelea.
Akizungumzia hali hiyo, Katibu wa Ulinzi wa Rasilimali za Ziwa
Victoria (BMU), Samson Pamba, alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kusema
tayari wameweka utaratibu wa kuwaadhibu wachafuzi na waharibifu wa
mazingira kwa kuwatoza faini ya sh 45,000 kwa atakayekamatwa.
Alisema tatizo hilo bado ni kubwa kutokana na baadhi ya watu
kuvunja sheria kwa makusudi, hali ambayo imekuwa ikisababisha wananchi
wengi wa eneo hilo kuugua magonjwa ya kuhara, kutapika, kutokana na
mazingira kuwa machafu.
“Wananchi wa eneo hili wamekuwa wakitumia maji ya Ziwa Victoria
kuoga, kufulia, kuoshea vyombo na wakati mwingine baadhi yao hutumia
maji hayo kwa ajili ya kunywa licha ya kwamba kuna visima ya maji ya
kunywa,” alisema.
Wanahabari walishuhudia pia shughuli za uchimbaji mchanga
kandokando mwa ziwa hilo zikiendelea licha ya mamlaka husika kusema
kuwa zilishapiga marufuku shughuli hizo.
0 comments:
Post a Comment