Azzan Zaungu |
MMOJA wa Wenyeviti wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa
Azzan Zungu pamoja na makada wengine wa CCM, juzi usiku walikamatwa na
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Dodoma kwa
tuhuma za rushwa.
Habari zilizopatikana mjini hapa juzi usiku zinasema, Zungu alikamatwa saa 4.30 katika moja ya vituo vya mafuta akidaiwa kujaribu kutoa rushwa ya Sh100,000 kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa uchaguzi wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM.
Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Eunice Mmari, jana alikiri kuwakamata baadhi ya watu wakijihusisha na vitendo vya rushwa akiwamo Zungu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mmari alidai kuwa vijana wake walimtia nguvuni Zungu juzi saa tatu usiku katika Hoteli ya Golden Crown akiwa na wapambe wake wakiendelea kugawa fedha kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Wazazi.
Alisema taarifa za Zungu kudaiwa kugawa fedha hizo walizipata juzi mchana na kuanza kufuatilia nyendo zake ambazo zilionyesha kuwa na dalili zote za rushwa.
“Tuliweka mitego yetu kila mahali ndipo tukabahatika kukutana naye katika eneo la hoteli hiyo akiwa na magari mawili, moja ikiwa ni teksi ya kawaida na nyingine ikiwa ni Prado ambayo ndiyo ilisadikiwa kubeba pesa,” alisema Mmari.
Kamanda huyo alidai kuwa kiasi cha fedha kilichokuwa kikitolewa na Zungu kilikuwa Sh100,000 kwa kila mjumbe ili kumshawishi ampigie kura.
Hata hivyo, alisema hawakuweza kumkamata moja kwa moja akitoa na hata fedha hizo hawakuzikamata kwani maofisa wa Takukuru walizingira gari dogo wakati fedha hizo zinasadikiwa zilikuwa katika Prado ambalo baada ya vurugu hizo lilitokomea kusikojulikana.
Akizungumzia madai hayo Zungu alisema: “Kwanza niseme kuwa si kweli kwamba nimekamatwa nikitoa rushwa, nilikuwa katika kituo kimoja cha mafuta wakaja watu ambao walisema wana shaka na gari langu.”
Aliendelea: “Samahani, halikuwa gari langu, bali ilikuwa ni teksi, mimi nikawaruhusu, wakaingia wakafanya ukaguzi na waliporidhika wakaniachia nikaondoka.”
Taarifa za awali
Zungu alikuwa mmoja wa wagombea wa nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) kupitia Wazazi katika uchaguzi uliofanyika jana mjini Dodoma.
Habari zilizopatikana mapema jana zilisema baada ya kukamatwa, Zungu alipelekwa Ofisi ya Takukuru Mkoa wa Dodoma ambako alihojiwa hadi saa nane usiku alipoachiwa baada ya kuwekewa dhamana na Mbunge wa Bukene (CCM), Selemani Zedi.
Habari hizo zinaeleza kuwa baada ya kukamatwa, gari alilokuwamo lilifanyiwa upekuzi kabla ya kupelekwa Ofisi za Takukuru, pamoja na makada wengine wa CCM ambao walikamatwa kwa tuhuma hizohizo.
Kamanda Mmari pia alithibitisha kukamatwa kwa makada wengine watano ambao aliwataja kuwa ni Yahaya Danga, Busuro Pazi na Frank Mang’ati ambao alidai kwamba walikuwa wakimsaidia Zungu katika mpango wake huo.
Mbali na watu hao, Takukuru ilimtia mbaroni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Mbeya, Fatuma Kasenga ambaye anadaiwa kukamatwa akitoa rushwa ya chakula kwa wajumbe.
Alisema alikamatwa katika Hoteli ya Kitoli, Barabara ya Iringa saa tisa usiku.
Alisema kuwa watuhumiwa hao kwa pamoja waliachiwa kwa dhamana na kwamba uchunguzi unaendelea.
Katika hatua nyingine, Mmari alisema kuwa taarifa walizokuwa nazo ni kuwa mgombea wa nafasi ya Uenyekiti wa Jumuiya hiyo, Abdallah Bulembo alikuwa akitoa rushwa zaidi.
“Tatizo ni kwamba wanazungumza lakini hawatoi ushirikiano, maana kama wangetoa ushirikiano tungeweza kuwakamata kwa urahisi,” alisema Mmari.
Bunge hawajui
Akizungumzia kukamatwa kwa mbunge huyo, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema Ofisi ya Bunge haikuwa na taarifa zozote kuhusu kukamatwa kwa mbunge huyo.
“Ndugu yangu, ndiyo nasikia kutoka kwako, sisi hatuna taarifa hiyo. Ni vigumu kuzungumzia jambo ambalo sijalisikia. Hata hivyo, nakushukuru sana kwa taarifa,” alisema Joel.
Rushwa CCM
Chaguzi za jumuiya za CCM zimekuwa zikilalamikiwa kugubikwa kwa vitendo vya rushwa na hata juzi baadhi ya wajumbe wa mkutano wa wazazi walilalamikia kuwapo kwa fedha nyingi kwenye uchaguzi huo.
Chaguzi nyingine zilizolalamikiwa kwa rushwa ni zile za Jumuiya ya Vijana (UVCCM) na Umoja wa Wanawake (UWT).
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akizungumza na wajumbe wa jumuiya hizo mbili kwa nyakati tofauti, alisema vitendo vya rushwa vinavyokithiri katika chaguzi za chama hicho, vinatishia uhai wake na kuwataka wanaCCM kubadilika.
Akifungua mkutano wa Jumuiya ya Wazazi jana, Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal pia alizungumzia rushwa: “Hakuna sababu ya kumchagua kiongozi kwa kuwa tu amekupa kitu kidogo! Hakuna sababu ya mgombea kuamini kuwa ukitoa hongo na rushwa ndiyo utachaguliwa.
“Muda wa kampeni umekwisha na sasa mmebakiza saa chache mpigiwe kura. Sitegemei kuwa mtawapa tena nafasi wapambe wenu kujihusisha na vitendo vya rushwa ndani ya ukumbi wa mkutano.”
Mmoja wa wajumbe alimwambia mwandishi wetu juzi usiku kwamba rushwa iliyokuwa ikitolewa ni Sh100,000 kwa kila mjumbe, lakini fedha hizo zilikuwa zikitolewa kwa awamu, ya kwanza walipewa Sh70,000, wakati kiasi kilichobaki cha Sh30,000 walitarajiwa kupewa jana.
Nje ya ukumbi
Eneo linalozunguka Ukumbi wa Chuo cha Mipango ulikofanyika uchaguzi huo, jana lilihanikizwa na nyimbo za hamasa kuanzia saa 1.30 asubuhi zikitoka kwa wapambe wa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi.
Wapambe hao walikuwa wakiimba na kuzunguka nje ya uzio uliozunguka ukumbi huo, huku wakiwa wamevalia fulana zenye picha za wagombea wanaowaunga mkono na kubeba mabango yenye picha za wagombea hao.
Msafara wa mgombea wa uenyekiti, John Barongo ulioongozwa na pikipiki, magari madogo kwa makubwa na basi lililokuwa na wafuasi wake, uliwasili na kulakiwa na kundi la vijana waliokuwa wakimuunga mkono. Katika msafara huo, alikuwapo kada mkongwe wa CCM, Mzee Job Lusinde.
Baadaye, takriban dakika saba hivi, uliwasili msafara wa mgombea mwingine wa kiti hicho, Martha Mlata na wapambe wake na baadaye msafara wa Bulembo, hali iliyosababisha eneo hilo la nje ya uzio kushindwa kukalika kutokana na pilikapilka za kampeni za dakika za mwisho.
Shamrashamra hizo zilikoma baada ya kuwasili kwa Dk Bilal ambaye alifungua mkutano huo, kisha kukabidhi kazi ya kuuendesha kwa wasimamizi wa uchaguzi ambao ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Zakia Meghji.
Habari tulizozipata wakati tukienda mitamboni zinasema, Bulembo alikuwa akielekea kushinda nafasi ya uenyekiti akiwaacha mbali wenzake Mlata na Barongo.
Katika nafasi ya makamu mwenyekiti, uchaguzi huo ulitarajiwa kurudiwa baada ya wagombea wote kutofikisha nusu ya kura.
chanzo cha habari: gazeti la mwananchi
0 comments:
Post a Comment