WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amekabidhiwa
ripoti ya uchunguzi wa utendaji kazi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), huku
akitoa onyo kali kwa vigogo waliokwepa kuhojiwa na kamati kwa visingizio
mbalimbali akisema ni lazima watahojiwa tu.
Dk. Mwakyembe alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya
kukabidhiwa ripoti hiyo yenye kurasa 285 na Mwenyekiti, Wakili Benard
Mbakileki, na kuongeza kuwa kama suala analotaka kuhojiwa mhusika linahusu
polisi, atapelekwa mbele ya jeshi hilo.
Waziri Mwakyembe alitoa kauli hiyo baada ya Wakili Mbakileki
kueleza kuwa baadhi ya watu muhimu TPA waliotakiwa kuhojiwa walikwepa kwa
visingizio mbalimbali ikiwamo kuuguliwa, kufiwa na wengine kuzima simu kabisa.
Akijibu hoja hiyo, Dk. Mwakyembe alisema: “Kama
walidhani kukwepa kamati ndio mambo yameisha, wanajidanganya. Watakuja kujibu
mbele yangu na kama mambo yanahusu polisi
tutawapeleka, hatutaacha mtu.”
Aliongeza kuwa kamati hiyo imefanya kazi ya kizalendo na
kuahidi mambo yote iliyopendekeza watayafanyia kazi hatua kwa hatua, ili
kuboresha bandari hiyo.
“Niwahakikishie hii kazi mliyoifanya haitakwenda bure, hadi
kufikia Desemba mwaka huu, tutakuwa tumeyafanyia kazi mambo yote
mliyopendekeza. Tutataka kuipa bandari sura mpya, kwa sasa inakosa
ufanisi…tutakuja na uamuzi ambao hakitadokolewa kitu, kwani watakaodokoa, nao
watadokolewa, kwani tusipofanya uamuzi huo hatutaikomboa nchi yetu,” alisema.
“Tulikuwa tunasikia habari za Twiga kusafirishwa kwenye
ndege watu wakashangaa, lakini pale bandarini kontena na ukubwa wake
linayeyuka. Mwaka juzi yaliyeyuka makontena 10, mwaka jana 26 na mwaka huu
mawili na mambo yanatufanya tusiaminike,” alisema.
Waziri Mwakyembe alibainisha kuwa kutokana na hali hiyo,
watafanya kazi kwa gharama yoyote, bila kumwonea mtu, ili kurekebisha bandari
hiyo aliyoeleza kuwa iwapo ingesimamiwa vizuri nchi ingeweza kuendesha mambo
mengi.
Aidha, alibainisha kuwa tangu kamati hiyo ilipoanza kufanya
kazi, baadhi ya nchi jirani zimeanza kurejesha imani na bandari hiyo zilikemo
Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, Rwanda na Burundi.
Aliongeza kuwa iwapo baadhi ya watu wanakerwa na mabadiliko
ndani ya TPA, waondoke kwani mjini kuna kazi nyingi za kufanya.
Pamoja na mambo mengine, Mwakyembe aliomba wapatiwe muda wa
kuipitia ripoti hiyo kwa umakini na kwamba kila hatua watakuwa wakitoa taarifa
kwa umma.
Kamati yanena
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mbakileki, alisema katika
kutekeleza uchunguzi waliwahoji watu 116 wakiwamo baadhi ya wajumbe wa Bodi na
Wafanyakazi wa TPA pamoja na uongozi wa Vyama vya Wanyakazi (Dowuta), Mamlaka
ya Mapato (TRA) Makao Makuu na kuonana na Kamishna Mkuu.
“Pia tulionana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo
(WMA) na maofisa wengine, eneo la Upakuaji na Upakiaji Mafuta (KOJ), Ticts na
kuonana na Meneja Mkuu na maofisa wengine pia kujionea utendaji kazi.
“Polisi Chang’ombe tulikutana na Mkuu wa Polisi wa Mkoa wa
Temeke, Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Temeke na maofisa wengine, kuzungumzia
kukamatwa kwa magari yanayobeba mafuta machafu bandarini pamoja na jaribio la
wizi wa kompyuta lililofanywa katika kituo cha WMA bandari kwa lengo ovu la
kupoteza ushahidi,” alisema.
Alieleza kuwa wadau wengi walijitokeza bila kutarajia, wengi
wao wakiwa na hamu ya kurudia mara mbili na pia mahojiano kwa mtu yalichukua
muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa ambapo mtu mmoja alihojiwa kati ya dakika 50
hadi 180, hali iliyochangia mahojiano kufanyika hadi saa sita usiku.
Pia alieleza kuwa walipitia nyaraka mbalimbali zikiwemo
sheria mbalimbali au Katiba ya nchi, Sheria ya TPA, sheria ya Mashirika ya Umma
na mikataba mbalimbali.
Wajumbe wengine wa kamati hiyo ni Ramo Makani (Makamu
Mwenyekiti), John Wanga, Halima Mamuya, Saidi Sauko, Richard Kasesela na
Bernardina Mwijarabu.
Alisema katika utendaji wao kazi walisimamia nguzo moja kuwa
‘Ukweli na haki ndio utakaotuweka huru’ katika kulinda na kuendeleza rasilimali
muhimu kwa maendeleo ya taifa.
Agosti 23, mwaka huu, Mwakyembe alitangaza kumsimamisha kazi
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Ephraim Mgawe, na viongozi wengine watatu, ili kupisha
uchunguzi wa tuhuma mbalimbali za ufisadi zinazowakabili. Nafasi ya Mgawe kwa
sasa inakaimiwa na Madeni Kipande kutoka Wizara ya Ujenzi.
Mbali ya Mgawe, vigogo wengine waliosimamishwa kazi ni
wasaidizi wake wawili, Julius Mfuko na Hamad Koshuma pamoja na Meneja wa
Bandari ya Dar es Salaam, Casian Nghamilo.
Baada ya kuwasimamisha viongozi hao, waziri huyo aliunda kamati
hiyo na kuipa hoja 34 ambazo ziliundiwa hadidu za rejea tisa, ili kuchunguza
chanzo cha kuzorota huduma TPA, hali inayochangia kukimbiwa na wateja wa ndani
na nje ya nchi.
CHANZO: TANZANIA DAIMA.
0 comments:
Post a Comment