CHAMA cha Alliance for Demokratic Change
(ADC), kimewalipua Rais Jakaya Kikwete na mtangulizi wake, Benjamin
Mkapa, kwa madai kwamba wamehodhi rasilimali nyingi za taifa kwa
maslahi yao binafsi na familia zao, kinyume cha taratibu na sheria za
nchi.
Katika utawala wake, Mkapa aliweza kujimilikisha shamba kubwa la
miwa la Mtibwa huko Morogoro pamoja na mgodi wa makaa ya mawe wa
Kiwira, huku Rais Kikwete akituhumiwa kuhodhi rasilimali za madini.
Akihutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Igoma jijini
Mwanza juzi, Katibu Mkuu wa ADC, Lucas Limbu, alisema umaskini
uliokithiri nchini unatokana na watawala kujali maslahi yao binafsi
badala ya taifa.
Alisema kuwa kitendo cha Rais Kikwete kushindwa kufumua mikataba ya
kifisadi katika sekta ya madini ni kielelezo tosha kwamba na yeye ana
maslahi katika mikataba hiyo.
“Watanzania tunalalamika mikataba ya madini ni mibovu. Lakini Rais
Kikwete amekaa kimya. Hawa watu wamejipanga kunyonya rasilimali za
taifa. Mkapa akiwa madarakani aliingiza marafiki zake Ikulu ili
wanyonye nchi. Alijimilikisha mgodi wa Kiwira na shamba kubwa la miwa
la Mtibwa. Kwa hiyo ADC inawaomba Watanzania waichukie na wainyime kura
CCM mwaka 2015,” alisema.
Katika mkutano huo zaidi ya wanachama 200 walijiunga na chama hicho
kwa kukabidhiwa kadi mpya, huku kukiwa na upinzani mkali kutoka kwa
wafuasi wa CHADEMA, waliokuwa wakiitikia ‘Power’ kila ilipotamkwa
salamu ya ADC kwa kunyoosha vidole viwili vya alama ya ‘V’ juu.
Kwa upande mwingine, Limbu alimshukia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
akimtuhumu kushindwa kusimamia vema majukumu yake na kwamba kwa sasa
hawezi kumsimamisha kazi mkuu wa wilaya wala mkoa.
Alisema Pinda ni muoga wa kuchukuwa hatua, huku akitolea mfano
sakata la aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David
Jairo, aliposhindwa kumwajibisha bungeni baada ya kudaiwa kukusanya
fedha kinyume na utaratibu.
Limbu alifafanua kuwa ADC ikiingia madarakani itahakikisha
inasimamia na kuboresha zaidi sekta ya elimu na kuwa mradi wa kwanza wa
serikali yake, kwani kwa sasa sekta hiyo imetelekezwa wakiwemo walimu.
Na Sitta Tuma-Mwanza
0 comments:
Post a Comment