Mhe. Christopher Ole Sendeka alipokuwa akiongea na waandishi na waandishi wa habari
MBUNGE wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara
Christopher Ole Sendeka amesema watu wote ambao nyumba na mali zao zilikutwa na
barabara ya Kia-Mirerani ambayo inatarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami watalipwa
fidia.
Ole Sendeka aliyasema hayo juzi wakati
akizindua kikundi cha wafanyabiashara wa madini ya Tanzanite cha Tupendane
Family kilichopo mji mdogo wa Mirerani ambapo zaidi ya sh6.2 milioni
zilipatikana katika uzinduzi huo.
Alisema Serikali imeshatenga fedha za awali za
ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami na miongoni mwa fedha hizo
zitatumika kuwalipa fidia wote ambao barabara iliwakuta wameshajenga nyumba zao.
“Barabara imeshatengewa fedha za ujenzi wa
awali na Waziri John Magufuli na nilipoomba ijengwe nilifikisha suala la fidia
hadi kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda hivyo hilo lisiwape wasiwasi,” alisema Ole
Sendeka.
Akizungumza na wanachama wa kikundi cha
Tupendane Family,mbunge huyo ambaye alisajiliwa rasmi kuwa mwanachama wa
kikundi hicho alisema kikundi hicho kitaweza kuwainua kupitia Saccos au Vicoba.
Alisema kuwa kikundi hicho kina dhamira na
malengo mazuri ya maendeleo kwa kujiinua kiuchumi,zaidi ya kusaidia wagonjwa au
waliofiwa na kina sura ya kitaifa kutokana na kuwa na jamii ya makabila
mbalimbali hapa nchini.
Naye,Katibu wa kikundi cha Tupendane Family
Dickson Nakembetwa alisema kikundi chao kilianzishwa mwaka 2010 kikiwa na
wanachama 30 na sasa kina wanachama 74 na wana akiba ya sh3 milioni kwenye
benki ya NMB.
Nakembetwa alisema lengo la kuanzishwa kwa
kikundi hicho ni kusaidiana wakati wa matatizo na hadi hivi sasa wanakikundi
saba wameshasaidiwa matatizo mbalimbali waliyonayo kwa kutumia sh1.1 milioni.
Alisema kiingilio cha kikundi ni sh20,000 ada
ya mwaka ni sh2,000 na hivi sasa wana mpango wa kutanua kikundi chao kwa
kuanzisha biashara na wanahitaji sh200 milioni kwa ajili ya kuanzisha miradi
mbalimbali ya maendeleo.
Na joseph lyimo-Manyara
|
0 comments:
Post a Comment