TAHADHARI YA UGONJWA WA MARBURG
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imepokea
taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), tarehe 20 Oktoba, 2012 kuhusu
ugonjwa wa Marburg ambao umejitokeza katika nchi jirani ya Uganda. Maeneo
yaliyokumbwa na ugonjwa huo ni Wilaya ya Kabale, Kanda ya Kusini Magharibi ya
nchi, na wilaya hii inapakana na Rwanda . Mpaka tarehe 24 Oktoba
2012, takriban watu 13 wamepata maambukizo na 6 wamepoteza maisha..
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda
kutoa tahadhari ya Ugonjwa huu kwa wananchi wote, katika mikoa yote ya Tanzania na hasa wale waliopo katika mikoa
ambayo inapakana na na nchi jirani ya Uganda (Mikoa ya Mara, Mwanza,
Kagera na Kigoma).
Chanzo kamili cha virusi vya ugonjwa huu hakijulikani. Hali inayosababisha
mlipuko wake pia haijulikani. Ugonjwa huu hauna tiba wala chanjo.
Dalili
kuu za ugonjwa huu
ni
pamoja na Homa kali, inayoambatana na kutokwa damu katika matundu yote ya mwili
yaani pua, njia ya haja kubwa na ndogo, mdomoni, masikioni, machoni, hali
inayopelekea kifo kwa muda mfupi. Kipindi cha kuonekana kwa dalili za
ugonjwa ni kati ya siku 3 hadi 9 baada ya kupata maambukizi.
Ugonjwa huu unaenea kwa urahisi sana na haraka
kutoka mtu mmoja hadi mtu mwingine iwapo mtu atakuwa karibu na mgonjwa na
kugusana na mate, damu, mkojo, machozi, kamasi, maji maji mengine ya mwili,
ikiwa ni pamoja na jasho au kumgusa mtu aliyekufa kwa ugonjwa wa Marburg.Ugonjwa huu pia unaweza kuenezwa iwapo mtu atagusa
nguo au mashuka ya mgonjwa wa Marburg.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imechukua
hatua zifuatazo katika kukabiliana na tishio la ugonjwa huu:
- Kutoa
taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu kupitia kwa Waganga Wakuu wote wa
Mikoa na Wilaya. Aidha taarifa hii pia imejumuisha namna mgonjwa anavyoweza
kutambuliwa (Ainisho la Ugonjwa), “Fact sheet” ya ugonjwa, Mwongozo
kwa watumishi wa afya wa namna ya kuchukua sampuli na vipeperushi
vinavyoelezea ugonjwa huu.
- Kuimarisha
ufuatiliaji wa ugonjwa huu kupitia kwa Wataalamu wa Afya katika Mikoa,
Wilaya na maeneo ya mipaka. Aidha watalaamu hawa wa Afya pia wanatoa elimu
kwa wananchi kuhusu dalili za ugonjwa huu ili endapo ugonjwa huo utatokea
uweze kutolewa taarifa mapema.
- Kupeleka
vifaa kinga kwa ajili ya watumishi wa afya
Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu kwani
mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote aliyeripotiwa nchini. Wananchi wanashauriwa
kutoa taarifa kwenye kituo cha huduma za afya kilicho karibu mara watakapoona
mgonjwa yeyote atakayehisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huu.
Taarifa
hii imetolewa na Kitengo cha mawasiliano ya Serikali
0 comments:
Post a Comment