MKUTANO wa Tisa wa Bunge la Muungano unatarajia kuanza kesho
Mjini Dodoma, huku ripoti ya Kamati Ndogo ya Bunge iliyoundwa kuchunguza tuhuma
za rushwa kwa baadhi ya wabunge ikisubiriwa kwa hamu kubwa.
Tume hiyo inayoongozwa na Hassan Ngwilizi iliundwa na Spika
wa Bunge, Anne Makinda kwa ajili ya kuchunguza tuhuma hizo zilizoibuka katika
mkutano wa Bunge uliopita. Tuhuma hizo ndizo zilizomfanya Spika kuivunja Kamati
ya Bunge ya Nishati na Madini.
Baada ya kuibuka kwa tuhuma hizo, Agosti mwaka huu, Makinda
aliunda tume ya wabunge watano kuchunguza tuhuma hizo.
Ripoti hiyo inatarajiwa kuwa mtihani mkubwa kwa Spika
Makinda hasa ikizingatiwa kwamba ndiye mwenye mamlaka ya kuwasilisha ripoti
hiyo bungeni hasa kutokana na kuibuka kwa maneno ya chinichini kwamba kumekuwa
na jitihada za kuwasafisha wabunge hasa wa chama tawala.
Hivi karibuni, Naibu Spika, Job Ndugai alikaririwa akisema
kuwa mamlaka ya namna ya kuiwasilisha ripoti hiyo yako mikononi mwa Spika
Makinda.
“Kwa kawaida na kanuni zetu ni kwamba Spika anaweza kuamua
kama ripoti hiyo ijadiliwe au iwasilishwe kwa njia ipi, wala hawezi
kuingiliwa,” alisema Ndugai.
Mbali na ripoti hiyo, Mkutano huo wa Bunge ambao utadumu kwa
wiki mbili, pia unatarajiwa kupokea hoja binafsi kutoka kwa Mbunge wa Kisarawe
(CCM), Suleiman Jaffo kuhusu mifuko ya jamii.
Jaffo aliibua hoja hiyo katika mkutano uliopita akitaka
itungwe sheria ya kufanya marekebisho ili kipengele kinachomtaka mwanachama wa
mfuko kupewa mafao yake pindi anapofikisha umri wa miaka 55 kiondolewe.
Wakati huohuo, Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Umoja
wa Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi walianza kuwasili Dodoma jana tayari kwa
mkutano wa uchaguzi unaotarajia kuanza kesho.
Awali, mkutano huo uliokuwa ufanyike Oktoba 27 hadi 28,
lakini ulisogezwa mbele ili kupisha waumini wa dini ya Kiislamu kuungana na
wenzao duniani kusherehekea Sikukuu ya Idd El Haj.
Katika uchaguzi huo nafasi ya mwenyekiti inagombewa na
Abdallah Bulembo na John Barongo na Martha Mlata.
Tayari Jumuiya nyingine za CCM za Umoja wa Vijana (UVCCM) na
UWT zimeshafanya uchaguzi wa viongozi wake wa juu wa kuziongoza kwa kipindi cha
miaka mitano.
(MWANANCHI)
0 comments:
Post a Comment