AZAM FC iko katika mpango wa kubadilishana wachezaji na Simba
SC, inataka Sh. Milioni 10 pamoja na kiungo Uhuru Suleiman kutoka kwa Wekundu
hao wa Msimbazi, ili wawape beki Mganda Joseph Owino.
Na Mahmoud Bin Zubeiry |
Tayari makubaliano yamefikiwa baina ya klabu hizo mbili,
ingawa Simba inaonekana kusuasua kutekeleza makubaliano hayo na hiyo pengine
inachangiwa na hali yao ya sasa si shwari.
Azam wanadai wamekubaliana na Simba walipe fedha hizo Sh
Milioni 10 na kumuidhinisha Uhuru kuhamia Chamazi, lakini suala la fedha bado
halijatekelezwa.
Inadaiwa hapo ni mbali na kesi ya fedha nyingine, Sh. Milioni
5, ambazo Simba wanadaiwa na Uhuru, ambazo Azam wamekubali kumpa fedha hizo
kiungo huyo halafu wao watawakata Simba kwenye mapato ya mlangoni katika mechi
ya marudiano ya Ligi Kuu baina ya timu hizo mwakani.
Mwishoni mwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, Azam
iliwasimamisha wachezaji wake watatu, kipa Deo Munishi ‘Dida’, mabeki Said
Mourad waliowahi kuchezea Simba, Erasto Nyoni na Aggrey Morris kwa tuhuma za
kuhujumu timu hiyo katika mchezo dhidi ya Wekundu wa Msimbazi, Oktoba 27, mwaka
huu ambao Wana Lamba Lamba walilala 3-1.
Baada ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati,
Kombe la Kagame Julai mwaka huu, Azam ilimuuza kwa mkopo kiungo Mrisho Khalfan
Ngassa ‘kwa hasira’ baada ya mchezaji huyo kubusu jezi ya timu yake ya zamani,
Yanga wakati wa Kombe la Kagame.
Azam walimuuza Simba Ngassa na siku chache baadaye, wakamuuza
Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kwa timu yake ya zamani, Simba SC.
MRISHO NGASSA:
Alisajiliwa kutoka Yanga kwa dau kubwa tu, lakini haikuchukua
muda akaanza kama kutoaminika anapocheza dhidi ya timu yake hiyo ya zamani,
kwamba hataki kuidhuru kutokana na mapenzi yake kwa timu hiyo. Iliendelea hali
hiyo hadi ilipofika Julai mwaka huu, alipowadhihirishia mapenzi yake kwa Yanga
kwa kuibusu jezi ya wana Jangwani, ndipo akauzwa Simba SC.
RAMADHANI CHOMBO:
Huyu alisajiliwa kutoka Simba SC kwa dau kubwa tu na mwanzoni
mwa msimu uliopita alitoroka kwenda Msumbiji kabla ya kukwama Hati ya Uhamisho
wa Kimataifa (ITC), hivyo kurejea Azam ambako alicheza hadi mwisho wa msimu.
Lakini Agosti mwaka huu, akajitoa Azam na kwenda kusaini Simba. Azam ilileta
tafrani kidogo, lakini baadaye ikaamua kumalizana na Simba ili mchezaji huyo
arejee timu yake ya zamani.
JOSEPH OWINO:
Alisajiliwa Azam akiwa majeruhi na klabu hiyo mbali na kumpa
donge nono la usajili, walimgharamia matibabu na wakamvumilia kukaa nje ya
Uwanja kwa msimu mzima klabla ya msimu huu kupona na kusajiliwa rasmi. Hata
hivyo, kocha Muingereza Stewart Hall hakuridhika naye na hakumpa nafasi katika
Kombe la Kagame na hata kocha aliyekuja baada yake, Mserbia Boris Bunjak naye
pia hakuridhishwa naye akawa anamsahau benchi. Stewart aliporejeshwa mwishoni
mwa mzunguko wa kwanza, bado aliendelea kutoona umuhimu wa beki hiyo Mganda,
hatimaye sasa anatolewa kuerejea klabu yake ya zamani.
SAID MOURAD:
Alisajiliwa kutoka Kagera Sugar, baada ya awali kuitumikia
Simba SC na alifikia kuwa beki tegemeo na kipenzi cha mabosi wa timu hiyo kwa
uadilifu na utendaji wake mzuri wa kazi, kiasi kwamba katika sherehe za msimu
za klabu hiyo Mei mwaka huu alipewa tuzo.
Lakini ghafla ikaibuka tuhuma kwamba, alihusika kuihujumu
timu hiyo katika mechi dhidi ya Simba SC. Wakati bado Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) inalifanyia kazi suala hilo, vigumu kuzama ndani
katika sakata lake, hadi hapo taarifa rasmi ya uchunguzi itakapotolewa.
DEO MUNISHI ‘DIDA’
Alisajiliwa kutoka Mtibwa Sugar msimu huu, baada ya awali
kutumikia Simba SC na alifikia kuwa kipa wa kwanza wa kuaminiwa na klabu hiyo,
chini ya makocha wote walioinoa Azam yeye akiwa kikosini, Muingereza Stewart
Hall na Mserbia Boris Bunjak. Lakini ghafla ikaibuka tuhuma kwamba, alihusika
kuihujumu timu hiyo katika mechi dhidi ya Simba SC. Wakati bado Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) inalifanyia kazi suala hilo, vigumu
kuzama ndani katika sakata lake, hadi hapo taarifa rasmi ya uchunguzi
itakapotolewa.
AGGREY NA NYONI:
Hawa hawajawahi kuchezea Simba na Yanga, lakini inawezekana
iwe wamehusika au la, lakini wanaingizwa au wanaingia kwenye mkumbo huu pengine
kutokana na kuwa kwao karibu na wachezaji waliowahi kuchezea vigogo hao wa soka
nchini. Wakati bado Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
inalifanyia kazi suala hilo, vigumu kuzama ndani katika sakata lao, hadi hapo
taarifa rasmi ya uchunguzi itakapotolewa.
AZAM IFIKIRIE UPYA KUSAJILI WACHEZAJI WA SIMBA NA YANGA…
Ukitazama historia utaona wachezaji wanaosajiliwa Azam ambao
walitoka Simba na Yanga, au waliwahi kuchezea timu hizo, wanafikia kuwa tatizo.
Ndiyo, Ngassa alikuwa tatizo kwa sababu aliwakosea Azam kwa kwenda kuibusu jezi
ya Yanga, nani anabisha hilo?
Redondo alikuwa tatizo, kwa nini aliitoroka Azam akiwa ana
mkataba na kwa nini akaenda kusaini SImba akiwa bado ana makataba?
Jiulize, wachezaji hawa walikuwa wanakosa nini Azam? Lazima
kuna kitu walikuwa wanakosa. Lazima. Hata yale mazoea ya kucheza wakishangiliwa
na maelfu ya mashabiki wa timu hizo, wakiikumbuka linaweza kuwa tatizo kwao. Au
hata staili ya malezi ya Simba na Yanga, kama waliipenda na wakawa wanaikosa
Azam, linaweza kuwa tatizo pia.
Kwa Mourad na Dida, hawa bado wanatuhumiwa, lakini suala lao
lina picha mbili, ambazo zote zinaifanya Azam ijitahidi kuachana na wachezaji
wa Simba na Yanga. Inawezekana wachezaji hawa hawahusiki kabisa na kuhujumu
timu, lakini wakawa wanatiliwa shaka kwa sababu wamewahi kucheza Simba. Lakini
pia kutokana na ukweli kwamba, mchezo huo mchafu upo katika soka ya Tanzania,
inawezekana pia tuhuma hizo zikawa kweli. Tusubiri ripoti rasmi ya uchunguzi
tupate ukweli.
Azam sasa hivi ni timu kubwa na japo haina mashabiki wengi,
lakini imezungukwa na watu wengi ambao kila mmoja ana hisia zake.
Kama watu wema au wabaya kwa Azam, kwanza kabisa ni watu
walio karibu na Wakurugenzi wa Bodi ya Azam. Hao ndio wanaotoa mawazo ya
kuijenga au kuibomoa Azam na kama tunaona hivi sasa Azam inakwenda vizuri, basi
sifa ziwaendee hao washauri wa Wakurugenzi kwa sasa.
Lakini pia kama tunaona mambo hayaendi vizuri kwa Azam hivi
sasa, basi lawama ziwaendee hao washauri
wa mabosi kwa sasa- lazima mawazo yao yatakuwa mabaya.
Siku inatoka taarifa ya kufukuzwa kwa akina Dida, Nyoni,
Mourad na Aggrey nilijiuliza, kwa nini Azam wamefanya hivi?
Hata kama kweli wachezaji hao walihujumu timu, basi biashara
si iliisha kwa mechi hiyo, kwa nini wasisubiriwe wamalize mechi na Mgambo JKT
wakaipa ushindi timu, kisha hata wakichukuliwa hatua, klabu itakuwa na fursa ya
kusajili mabeki wengine. Lakini wakafukuzwa na kwa timu kukosa mabeki, ilibidi
watu wachezeshwe katika nafasi ambazo si zao na ninaamini hiyo ilichangia
kipigo cha Mgambo. Sijui Azam ilipoteza pointi moja au tatu katika mechi hiyo,
lakini leo isingekuwa inazidiwa pointi tano na Yanga.
Kuna maamuzi ambayo hayatokani na kujifikiria mara mbili
ndani ya Azam na ndiyo maana Stewart alifukuzwa, akarejeshwa.
Sasa basi, kutokana na hali ilivyo, je bodi ya Wakurugenzi ya
Azam na Menejimenti kwa ujumla, haioni ni bora ikatengeneza mazingira ya
kuepuka matatizo kutokana na uzoefu waliokusanya katika kipindi cha miaka
mitano ya kuwapo kwao Ligi Kuu?
Waachane na wachezaji wa Simba na Yanga. John Bocco
‘Adebayor’ ni mchezaji wa Azam ambaye anaaminika kwa sababu ametoka ndani ya
Azam kama ilivyo kwa vijana wengine,akina Himid Mao, Salum Abubakar na wengineo.
Azam wana Akademi bora, ambayo Abedi Pele alipokuwa nchini
aliisifia mno. Je, kwa nini sasa Bodi ya Ukurugenzi isitupie jicho hapo. Wakati
Pele alipotembelea Azam Complex, Chamazi kuna wakati tulijitenga mimi, Katibu
wa Azam, Nassor Idrisa na rais wa TFF, Leodegar Tenga tukawa tunajadili, kwa
nini Azam isifikie kuwaamini wachezaji wao wa Akademi na kuanza kuwapa nafasi
katika Ligi Kuu?
Wamekaa pamoja kwa muda mrefu wakipata mafunzo na malezi
mazuri. Wengi wao ndio wanaotegemewa katika timu za taifa za vijana.
Ipo haja ya Azam pamoja na utajiri wake ikajitofautisha na
Simba na Yanga. Simba na Yanga wakisajili kila msimu huwezi kuwastaajabu kwa
sababu hawana akademi. Lazima ifike wakati watu waone matunda ya akademi ya
Azam.
Inasikitisha mno Azam kuanza kuingia kwenye migogoro
iliyozoeleka Simba na Yanga mapema namna hii. Lazima Azam iwe tulivu.
Watanzania wengi wanatarajia makubwa kutoka Azam. Hata Pele ametabiri siku
moja, Azam itakuwa klabu kubwa kama za Ulaya, akitolea mfano Manchester United
ya England. Akasema ana mengi ya kujifunza kutoka Azam.
Wapo watu mji huu, wanaishi kwa maneno tu, kazi yao
kujipenyeza penyeza ili wauze maneno wapate riziki. Je, wangapi kati yao
wamejipenyeza Azam na hayo maneno wanayouza yanaijenga na kuibomoa Azam kwa
kiasi gani? Haya ni mambo ambayo Bodi ya Wakurugenzi ya Azam inapaswa
kuyaangalia kwa makini. Jamani, kwa leo inatosha! Alamsiki.
0 comments:
Post a Comment