.

.
Monday, November 26, 2012

8:33 PM
Msanii maarufu wa Luninga, Sharo Milionea (pichani), amefariki dunia leo katiak ajali ya gari iliyotokea kijiji cha Lusanga, Muheza, mkoani Tanga.
Marehemu Sharo Milionea

MSANII wa filamu, Hussein Mkiety a.k.a Sharo Milionea amefariki usiku wa leo kufuatia ajali ya gari iliyotokea eneo la Maguzoni, Songa, Muheza.

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi wa mkoa wa Tanga,
Constatine Masawe, Sharo alikuwa peke yake garini wakati ajali hiyo ikitokea na mwili wake uko katika hospitali ya Teule, Muheza. 


Kamanda Masawe alisema Milionea akiwa anaendesha gari namba T478 BVR Toyota Harrier akitokea Dar es Salaam kwenda Muheza alipofika eneo hilo gari lake liliacha njia na kupinduka mara kadhaa na kusababisha kifo chake.


Hii ni ajali ya pili kwa Sharo kupata mwaka huu baada ya Januari 5 kunusurika katika ajali ya basi alilokuwa amepanda la Taqwa likitokea Burundi kuelekea Dar es Salaam kupinduka katika eneo Mikese, Morogoro saa mbili na nusu asubuhi.

Sharo ambaye alikuwa amekaa kwenye siti ya mbele kabisa alipoteza simu tu katika ajali hiyo ambayo ilijeruhi abiria wengine vibaya.


Kifo cha Sharo kinafuatia vifo vya wasanii wengine wawili wa filamu nchini ndani ya wiki moja, Mlopelo aliyetamba na kundi la Kaole na John Maganga aliyetamba na filamu ya 'Mrembo Kikojozi' aliyocheza na Aunt Ezekiel. 

Vifo hivyo vinakumbushia msiba wa Steven Kanumba, ambaye pia alifariki ghafla. 

Sharo atakumbukwa kwa ubunifu wake katika uigizaji akitoka kama mchekeshaji msafi tofauti na wachekeshaji wengi waliomtangulia ambao waliamini vichekesho ni lazima kuvaa kama katuni, kujaza nguo tumboni ili kuonekana na matumbo makubwa ama kujipaka masizi.

Akipendeza kwa mavazi nadhifu, Sharo Milionea alipata umaarufu kwa msemo wake wa "kamata mwizi meeen" na "Ooooh mamma!" huku akijipangusa mabega katika pozi za kibrazameni.

Katika siku za karibuni amekuwa akitawala vioo vya televisheni kutokana na kushiriki tangazo la kampuni ya huduma za simu ya Airtel akiwa na mchekeshaji mkongwe King Majuto, ambapo msemo wake mwingine wa "umebugi meen!" umetawala hasa midomoni mwa watoto.

      


Marehemu Mlopelo
Marehemu Steven Kanumba

BERTHA BLOG imeguswa na msiba huo na kwa kutambua umuhimu wa sanaa hapa nchini inawapa pole ndugu jamaa marafiki na wasanii wenzake ikiwemo Watanzania wote kwa ujumla walioguswa na msiba huo.
 
BWANA AMETOA, BWANA AMETWAA JINA LA BWANA LIHIMIDIWE 
AMINA

0 comments:

Post a Comment