Virusi wa Ebola
Maafisa
afya nchini Uganda wamesema kwamba watu watatu wamekufa baada ya kuugua
ugonjwa wa Ebola, lakini serikali haina uhakika kuhusu kilichosababisha
visa hivi vilivyotokea Luweero.
Inashukiwa
kuwa watu wengine watano wameambukizwa,wawili kati yao wametengwa
katika wodi maalum katika hospitali kuu ya Mulago, mjini Kampala.
Hii ni mara ya tano kwa kuzuka kwa Ebola nchini humu katika miaka 12 iliyopita.
Mlipuko wa ugonjwa huo mnamo Julai mwaka huu ulisababisha vifo vya watu 17.
Inakadiriwa kuwa watu 17 waliaga dunia magharibi mwa Uganda, kutokana na ugonjwa huo mwezi Julai mwaka huu.
Kwa
mujibu wa shirika la madaktari wasio na mipaka la Medecins Sans
Frontieres (MSF), hakuna maafa yoyote yaliyoripotiwa kuhusiana na
ugonjwa huo hatari tangu mwezi Agosti.
Waziri
huyo wa Afya ameliambia shirika la habari la AFP, kuwa uchunguzi
uliofanywa umethibitisha kuwa watu hao waliaga dunia kutokana na
ugonjwa huo wa Ebola katika eneo la Luwero, takriban kilomita sitini
kutoka mki mkuu Kampala.
Lakini amesema
mwanaume mmoja kutoka eneo hilo, pia aliaga dunia mwezi uliopita,
kutokana na kile kilionekana kuwa dalili za ugonjwa huo, lakini hakuna
uchunguzi uliofanyika kuhusiana na kifo hicho.
Watu
watano ambao ni jamaa wa karibu wa walioaga dunia, wanaendelea
kuchunguzwa na madaktari. Wawili kati yao wamelazwa katika chumba
maalum katika hospital kuu ya kitaifa ya Mulago mjini Kampala.
Hakuna
tiba maalum inayojulikana ambayo inaweza kutumika kutibu ugonjwa huo,
lakini wagonjwa hupewa dawa za kawaida za kinga pamoja na zile za
kupunguza maumivu na kutibu Malaria ili kuongeza kinga mwilini.
Asilimia
Tisini ya watu wanaogunduliwa kuwa na virusi vinavyosababisha ugonjwa
huo wa Ebola huaga dunia, na katika kipindi cha miaka Kumi na mbili
iliyopita kumekuwa na visa kadhaa vya mkurupuko wa ugonjwa wa Ebola
nchini Uganda.
Takriban asilimia 50 ya yatu 425 ambao walikuwa wameambukizwa virusi hivyo waliaga dunia mwaka wa 2000.
Wizara
ya Afya, pamoja na Shirika la Afya Duniani walikuwa wametangaza kwamba
ugonjwa huo ulikuwa haupo tena Uganda. Lakini umezuka tena.
Wanaougua Ebola hupata homa kali, huvuja damu, na viungo vyao vya mwili vya ndani huacha kufanya kazi.
Waganda
wengi wanashangaa ni kwa nini nchi yao hukumbwa mara kwa mara, lakini
serikali inasema kwamba ni kwa sababu mifumo yao ya uchunguzi imeboreka
zaidi.
Hali kadhalika, katika mwezi mmoja
uliopita watu tisa wamefariki baada ya kuugua ugonjwa wa homa
unaoambukiza wa Marburg, unaofanana na Ebola.
0 comments:
Post a Comment