JESHI
la Polisi mkoani Mbeya linawashikilia watu 10 wanaodhaniwa kuwa ni
askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kikosi cha 44 KJ Kambi ya
mji mdogo wa Mbalizi kwa tuhuma za mauaji ya mkazi wa mji huo, Petro
Sanga (25).
Askari hao wanadaiwa kumuua Sanga kwa kumchoma kisu
shingoni na mdomoni, kisha kuwajeruhi watu wengine sita kwenye Baa
iitwayo Power Night, ambako walikwenda kwa lengo la kulipiza kisasi cha
kupigwa kwa askari mwenzao, Geodfery Matete (30).
Hata hivyo,
Matete anadaiwa kwamba alikuwa amepigwa na walinzi wa kilabu cha pombe
cha DDC kilichopo katika mji huo wa Mbalizi, Novemba 18 mwaka huu saa 3
usiku.
Mauaji hayo yamekuja siku moja baada ya Mahakama Kuu
Kanda ya Dar es Salaam kuwahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa
askari watatu wa JWTZ na JKT, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua,
Swetu Fundikira.
Hata hivyo, askari hao waliohukumiwa kunyongwa,
jana waliwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa katika Mahakama
Kuu ya Tanzania.
Kamanda wa Polisi mkoani wa Mbeya, Diwani
Athuman alithibitisha mauaji hayo mapya yaliyotokea katika Mji wa
Mbalizi na kwamba marehemu Sanga alikutwa na mauti akiwa anakunywa
pombe kwenye baa iitwayo Power Night.
“Marehemu na wenzake
walivamiwa na askari hao na kuanza kuwashambulia. Askari hao
waliwashambulia wananchi waliokuwapo kwenye baa hiyo na Sanga alifariki
dunia baada kupigwa sehemu mbalimbali za mwili wake kwa mateke,
mikanda, marungu, sime na mapanga,” alisema Kamanda Athuman na kuongeza:
“Baada
ya kumpiga walimchoma kisu mdomoni. Katika jitihada zake za kujiokoa,
marehemu alikimbilia katika baa nyingine ya Vavenemwe.”
Kwa
mujibu wa Kamanda Athuman, baada ya marehemu kufika katika baa hiyo
alipoteza fahamu na wasamaria wema walimbeba na kumkimbiza katika
Hospitali Teule ya Ifisi iliyopo katika mji huo mdogo.
“Alifariki wakati akipatiwa matibabu na hiyo ilitokana na kuvuja damu nyingi,” alisema.
Chanzo cha vurugu
Kamanda
Athuman alisema chanzo cha vurugu hizo, ni askari wa JWTZ, Matete
(30) kushambuliwa na walinzi wa kilabu cha pombe za kienyeji
kilichojulikana kwa jina la DDC Novemba 17 mwaka huu.
Alisema
kuwa kutokana na tukio hilo, Polisi wanawashikilia walinzi wanne kwa
mahojiano zaidi ambao ni Frank Mtasimwa (25), Mure Julius (26), Omari
Charles (28) na Regnad Mwampete, wote wakazi wa Kijiji cha Izumbwe
Wilaya ya Mbeya.
Kamanda Athuman alisema majina ya askari
waliokamatwa kwa tuhuma hizo yatatajwa baadaye kwani bado uchunguzi
unaendelea huku akivitaka vyombo vya dola kuacha kujichukulia sheria
mkononi kwa kuwa hali hiyo inaweza kusababisha uvunjifu wa amani.
“Uchunguzi wa tukio hili ukikamilika waliokamatwa watafikishwa mahakamani” alisema.
Msemaji
wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe alisema kuwa hana taarifa za wanajeshi
hao kufanya mauaji huku akisisitiza kuwa kama wanashikiliwa na Jeshi la
Polisi ni wazi kuwa watakuwa wanahusika na tukio hilo.
“Bado
sijapata taarifa rasmi kuhusu tukio hilo kwa kuwa hivi sasa sipo katika
eneo la kazi, polisi ndio wanaweza kusema lolote na kama kweli
wanawashikilia basi watakuwa wamehusika,” alisema Mgawe.
Walioua na rufaa
Wakati
huohuo, askari watatu wa JWTZ, waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa baada
ya kupatikana na hatia ya kumuua Swetu Fundikira, jana wamewasilisha
taarifa ya kusudio la kukata rufaa katika Mahakama Kuu ya Tanzania.
Wakili
wa askari hao, Mluge Karoli alisema wamewasilisha kusudio hilo la
taarifa ya kukata rufaa kwa sababu hawajaridhishwa na uamuzi uliotolewa
na Jaji Zainabu Muruke wa kuwatia hatiani wanajeshi hao kwa kosa la
kumuua kwa makusudi Fundikira, kinyume cha kifungu cha 196 cha Kanuni
za Adhabu.
Karoli akitoa sababu za kuwasilisha kusudio hilo la
kukata rufaa alidai kuwa kesi yoyote ya ugomvi haiwezi kuwa na
kusudio la kutaka kuua na kwamba hakuna shahidi aliyefika mahakamani
hapo na kueleza kuwa wateja wake ndio wamemuua Swetu Fundikira.
Pia
alienda mbali zaidi na kudai kuwa wateja wake ambao ni MT 1900 Sajini
Roda Robert (42), MT 85067 Koplo Mohamed Rashid wa JKT Mbweni na MT
75854 Koplo Ally Ngumbe (37) wa kikosi cha JWTZ Kunduchi hawakuwa na
wajibu wa kuthibitisha mauaji hayo.
“Waliomuua marehemu Swetu
siyo wateja wangu na ninaamini Mahakama ya Rufani itaangalia upya
ushahidi na kutenda haki,” alidai Karoli.
Aliongeza kudai kuwa
aliyepambana na wateja wake ni Swetu Fundikira na uchunguzi wa daktari
unaonyesha jina la Swetu Ramadhani Fundikira hivyo ni watu wawili
tofauti na kwamba hakuna hata shahidi mmoja aliyesema aliwahi kuona
mwili wa marehemu ama kuhudhuria kwenye msiba.
Askari hao kwa
pamoja wanadaiwa kuwa walimpiga Fundikira, Januari 23 mwaka huu saa
7:30 usiku wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam na baadaye kufariki
dunia usiku huohuo wa kuamkia Januari 24, mwaka 2010, katika Hospitali
ya Taifa Muhimbili.
Hukumu hiyo iliyotolewa juzi na Jaji Mruke,
ilifufua upya msiba wa Swetu, baada ya ndugu zake kuangua vilio, huku
chumba cha Mahakama kikigeuka kwa muda kuwa sehemu ya msiba.
Sambamba
na vilio hivyo, ndugu wawili wa marehemu Swetu walianguka chini na
kuzirai kwa muda, kabla ya kupewa huduma ya kwanza na kurejea katika
hali ya kawaida.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Muruke alisema ingawa
hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa washtakiwa hao ndio waliomuua
Fundikira, ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka (Jamhuri) ulikuwa
ni ushahidi wa mazingira, kwamba Jamhuri imeweza kuthibitisha mashtaka
hayo.
Alisema kuwa anakubaliana na mtiririko wa ushahidi wa
upande wa mashtaka kama ulivyoelezwa na mashahidi wake sita akiwamo
daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu, askari polisi wawili
ambao washtakiwa katika utetezi wao walishindwa kuuvunja.
“Sheria
iko wazi ukiondoka na mtu au ukionekana naye kwa mara ya mwisho na
baadaye mtu huyo akapatikana na madhara, wewe ndio unawajibika kutoa
maelezo ya kina kuhusu yaliyompata mtu huyo” alisema Jaji Muruke na
kuongeza;
“Kisheria ukitoa maelezo ambayo hayajakidhi haja na
yana utata ni faida kwa upande wa mashtaka ambao hutegemea ushahidi wa
mazingira. Maelezo ya kina hayajatolewa na washtakiwa wote.”
Aliendelea,
“Ushahidi wa Jamhuri japokuwa ni wa mazingira, umejengwa thabiti na
upande wa utetezi haukuweza kujenga matundu, ama kuuvunja mnyororo
huo, kidole kinawaelekea wao.”
Jaji Muruke alisisitiza kuwa
katika kesi hiyo licha ya kuwa kuna ushahidi wa kimazingira, upande wa
mashtaka umeweza kuthibitisha mashtaka bila kuacha shaka.
“Hivyo
kosa wanaloshtakiwa nalo limethibitishwa na Mahakama imewaona
washtakiwa kuwa wana hatia ya kumuua Swetu Abdallah Fundikira” alisema
Jaji Muruke.
chanzo:mwananchi
0 comments:
Post a Comment