CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kuwa
kinafurahi kuona kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kinatekeleza sera
walizozianzisha wao.
Kauli ya CHADEMA ilitolewa na Katibu Mkuu wake, Dk. Willibrod Slaa,
wakati akifungua rasmi Baraza la Mashauriano la Mkoa wa Kagera ambalo
linaundwa na viongozi kutoka katika kila jimbo la mkoa huo,
linalofanyika kwa muda wa siku tatu katika wilaya ya Karagwe.
Dk. Slaa alisema CHADEMA waliwezesha kufutwa kwa kodi za manyanyaso
katika wilaya ya Karatu baada ya kulikalia kidete suala hilo, na ndipo
CCM ilitumia sera hiyo na kuondoa kodi za namna hiyo takriban nchi
nzima.
Aliongeza kuwa walianzisha pia sera ya kujenga zahanati kila kata
wilayani Karatu, ambayo nayo CCM baadaye ilichukua na kisha kutangaza
kuanzisha utaratibu wa kujenga zahanati kila kata nchi nzima.
“Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu 2010, CHADEMA tuliahidi sera ya
kupunguza gharama za vifaa vya ujenzi nchi nzima kama tungeingia
madarakani. Wakati huo CCM ilidai haiwezekani ila sasa nao wametangaza
kupunguza gharama za bidhaa hizo,” alisema.
Alifafanua ni wazi kuwa CCM ikiweza kutekeleza sera ya CHADEMA ya
kupunguza gharama za vifaa vya ujenzi na kutoa elimu bure kabla ya
mwaka 2015, watafurahi maana hawana wivu, lakini wakishindwa itakuwa
ndiyo njia yao ya kuondoka madarakani.
Dk. Slaa aliongeza kuwa CHADEMA haiwezi kuchukia kutokana na CCM
kutekeleza sera zake maana zinapotekelezwa wananchi wanapata mabadiliko
na unafuu wa maisha.
Alisema kuwa kelele zao zinahitaji uchumi wa nchi usimamiwe vizuri
na kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi wote, na kwamba mpaka sasa
inashangaza kuona CCM imeshindwa kupata majibu yanayosababisha wananchi
kuendelea kuwa maskini.
Dk. Slaa alichanganua kuwa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Nyerere, aliweza kuanzisha viwanda ambavyo sasa vingi vimefungwa, bila
kuchimba dhahabu na wala kuuza samaki nje ya nchi, lakini akahoji ni
kwa nini wakati huu ambao tunauza madini, samaki nje ya nchi maendeleo
yamedumaa.
“Mfano Waingereza hawana mashamba makubwa lakini hata siku moja
hawakuwahi kulia njaa. Sisi Tanzania tuna mabonde makubwa ambayo
yakitumiwa ipasavyo mawili yanaweza kutosha kulisha nchi nzima, lakini
bado tunalia njaa,” alisema.
Alibainisha kuwa kutokana na kutokuwa na mpangilio mzuri, mawazo
mgando yaliyopo hayawezi kuleta maendeleo. Alitolea mfano kuwa
inashangaza kuona bado tuna treni inayosafiri siku tatu kutoka Dar es
Salaam hadi Mwanza.
Katibu huyo aliwataka viongozi wa chama hicho kutoogopa kukemea
maovu yanayofanywa na baadhi ya viongozi walioko madarakani na kwamba
kiongozi bora lazima aonyeshe madadiliko katika eneo lake.
Alisema CHADEMA iko katika harakati za kuboresha na kuimarisha
utendaji kazi wa ndani kwa kununua pikipiki kila kata nchi nzima,
kuajiri makatibu na kutafuta ofisi za kudumu na zenye hadhi.
0 comments:
Post a Comment