Serikali
ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imetoa wito kwa Umoja wa Mataifa
kuichukulia hatua Rwanda, kwa madai ya kusaidia waasi nchini Congo
badala ya kumfuatilia mtu mmoja kama vile kanali Sultani Makenga.
Waziri
wa habari wa serikali ya Congo amesema hayo siku moja baada ya Umoja wa
Mataifa na Marekani kutangaza vikwazo dhidi ya kiongozi wa waasi wa
M23, Jenerali Makenga, vikiwemo vya usafiri na kukamata mali yake.
Serikali
ya Marekani pia imewazua Wamarekani kujihusisha kwa namna yoyote na
Sultan Makenga, ambaye alikuwa afisa wa ngazi ya cheo cha Jenerali
katika jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Hata
hivyo haijaeleweka iwapo hatua ya kukamata mali itakuwa na athari kwani
inadhaniwa kuwa Makenga huenda hana mali ya kiasi cha kumtisha ambayo
iko nchini Marekani.
Taarifa ya Umoja wa
Mataifa, imesema waasi wamekuwa wakipata silaha kinyume na amri ya
Umoja wa Mataifa inayozuia biashara ya silaha kuingia nchini humo.
Taarifa
hiyo pia imemtaja Jenerali Makenga kuhusika na vitendo vya mauaji,
ukataji viungo vya binadamu, ubakaji, utekaji nyara dhidi ya raia na
kuwalazimisha watu kuyakimbia makaazi yao.
Balozi
wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Susan Rice, amesema vikwazo vipya
vinaonyesha kuwa dunia haitavumilia vitendo vya uhalifu vilivyofanyika
chini ya amri ya Jenerali Makenga.
Uasi
ulianza mwezi March wakati wanajeshi waasi walipojitoa kutoka jeshi la
Congo na kutwaa miji karibu na Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu
Kaskazini mashariki mwa Congo.
Maafisa
walioasi walipinga kuhamishiwa katika maeneo mengi ya nchi wakisema
wanataka kubakia katika eneo la mashariki kwa madai ya kuwalinda
wananchi wa eneo hilo.
Pia wanasema wanataka wakimbizi wanaoishi Rwanda, Uganda na Burundi, kupelekwa katika eneo hilo.
Umoja wa Mataifa umezishutumu Rwanda na Uganda kwa kuwaunga mkono waasi, shutuma ambazo nchi zote mbili zimekana kuhusika.
chanzo cha habari:bbc
0 comments:
Post a Comment