.

.
Thursday, November 22, 2012

5:02 AM



KATIKA kile kinachoonekana ni kujaribu kutikisa ngome ya Chadema wilayani Arusha ,Chama Cha Mapinduzi(CCM) mkoani hapa kinataraji kufanya mkutano mkubwa wa hadhara  utakaoambatana na ufunguzi wa mashina mbalimbali ya wakereketwa wa chama hicho yakakayozinduliwa na katibu mkuu mteule wa CCM,Abdulrahaman Kinana.

Baadhi ya viongozi mbalimbali wa kitaifa wakiwemo wajumbe wapya wa sekretarieti ya CCM akiwemo katibu wa itikadi na uenezi,Nape Nnauye,naibu katibu mkuu wa CCM bara,Mwigulu Nchemba wanatarajiwa  siku chache zijazo mkoani Arusha kwa lengo la kuongoza mashambulizi ya kushambulia ngome hiyo.

Akiongea na waandishi wa habari leo jijini hapa,katibu wa siasa na uenezi wa CCM mkoani hapa,Isaac Joseph Kadogoo alisema kwamba mkutano huo utafanyika novemba 24 mwaka huu ambapo kutakuwa na maandamano makubwa ya kumpokea Kinana kuanzia uwanja mdogo wa ndege uliopo Kisongo jijini hapa hadi wilayani Arumeru na kisha kurejea katikati ya jiji la Arusha.

Kadogoo,alisema kwamba lengo la shughuli hiyo ni kumkaribisha Kinana ambaye ni mkazi wa mkoani Arusha sanjari na kuelezea sera mbalimbali yakiwemo maendeleo yaliyoletwa na CCM mkoani Arusha na nchini kwa ujumla.

Hatahivyo,katibu huyo wa siasa na uenezi alisema kuwa viongozi mbalimbali wa CCM taifa watapata fursa ya kuwahutubia wakereketwa wa chama hicho katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid sanjari na wakazi wa Arusha katika mkutano ikiwa ni pamoja na  kuongoza  uzinduzi wa matawi hayo.

Alisisitiza kwamba hadi sasa taratibu mbalimbali za maandalizi kwa ajili ya shughuli hizo yamekamilika kwa asilimia mia moja ambapo katika maandamano ya kumpokea Kinana kutakuwa na msafara  wa magari,pikipiki pamoja na watembea kwa miguu.

Hatahivyo,aliwataka wananchi wa CCM mkoani Arusha kujitokeza kwa wingi katika sherehe hizo huku akienda mbali na kudai kuwa kutakuwa na vikundi mbalimbali vya ngoma na wasanii watakaotumbuiza kusindikiza sherehe hizo.

Katika hatua nyingine,Kadogoo alijitamba kwamba Chama hicho kimejipanga kikamilifu kushinda katika uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Arusha mjini endapo mahakama kuu ya rufaa nchini ikitupilia rufaa iliyowasilishwa na mbunge wa zamani wa jimbio hilo,Godbless Lema.

“Naomba nieleweke kwamba CCM tumejipanga na kujidhatiti kushinda uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Arusha mjini endapo rufaa ya Lema ikitupiliwa mbali na mahakama kuu ya rufaa na ujio wa Kinana tunaamini utatikisa hapa mjini”alisema Kadogoo


0 comments:

Post a Comment