.

.
Tuesday, November 20, 2012

8:50 PM

Wakulima kote nchini wametakiwa kutoridhika na mazao yao badala yake kuongeza kiwango cha mazao na kipato kwa ujumla kwa kulima kwa kutumia kilimo cha kisasa ikiwemo kuandaa mashamba mapema kabla ya msimu wa mvua kuanza.

Rai hiyo imetolewa na meneja mkuu wa kiwanda cha mbolea ya minjingu bwana Anup Modha alipokuwa alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kwenye mkutano wa wadau wa kilimo uliofanyika hivi karibuni mkoani Arusha.

Bwana Anup alisema kuwa wakulima wengi kwa sasa wanalima kilimo cha mazoea kwa kupanda mazao bila kugeuza shamba wala kuweka mbolea sambamba na kumwaga mbegu bila kupangilia hali ambayo huwaletea hasara kwa kuvuna mazao kidogo isiyolipa jasho lake.

Alisema “hata hivyo pamoja na wakulima kupata mazao kidogo ambayo hata haitoshi chakula licha ya kubaki ya akiba kuuza, wamekuwa wakiridhika na hali hiyo na kutotaka kubadilika hali ambayo huwafanya kubaki kuwa masikini siku zote kwa kuwa na kipato duni wakati mazao yao ndio kila kitu katika nchi yoyote duniani.

Aliongeza “endapo mkulima atabadilika na kuzingatia kjilimo cha kisasa na watapata mazao mengi watakayotumia kwa chakula na biashara hali itakayowaongezea kipato na kuondokana na hali duni ya maisha” alisema Anup na kuongeza.

“Kufuatia hayo basi niwaombe tu wakulima wetu wanapokaribia msimu wa mvua waanze kwanza kugueza mashamba yao kwaajili ya maandalizi ya kupanda sambamba na kuweka mbolea ambapo kama wanapanda mazao mseto (kupanda zaidi ya zao moja kwenye shamba) basi wazingatie kupanda mazao zitakazorutubisha ardhi kama kuchanganya mahindi na maharage.”

Alisema kufanya hivyo kutasaidia mazao kuendelea kupata chakula cha kutosha kutoka ardhini ambapo mbolea husaidia mizizi ya mimea kuwa mikubwa na kuwa na uwezo wa kuchimba chini zaidi ya mita 3kujitafutia chakula chake ambapo pia huwa na uwezo wa kupambana na magonjwa na ardhini.

Mmoja wa washiriki katika mkutano huo wa wadau wa kilimo, Iddy Rajabu Chongi kutoka mkoa wa Kilimanjaro alisema kuwa ziko changamoto nyingi zinazowakabili wakulima hasa wa vijijini hali inayawafanya kukata tama na shughuli hiyo na matokeo yake kufanya kwa mazoea.

“Kiukweli shughuli za kilimo ni shughuli muhimu sana hapa nchini lakini bado serikali haijaipa kipaumbele sana kutokana na kukabiliwa na changomoto nyingi ikiwemo ya ukosefu wa soko la uhakika wa mavuno yetu” alisema Chongi na kuongeza.

“Mbali na hilo pia wakulima wengi wanategemea msimu wa mvua hali ambayo ukame ukiikumba nchi lazima wakulima  wafe njaa hali ambayo kama serikali ingefanya mpango wa kuboresha miundombinu ya umwagiliaji kwa wale wanaoishi karibu na miudombinu hiyo basi ingesaidia kuinua kiwango na kipato cha wakulima hapa nchini”

Alisema kuwa katika kijiji cha Gona kata ya kahe wilayani Moshi wao wanategemea zaidi kilimo mseto cha umwagiliaji ambacho kimekuwa na manufaa makubwa kwao kwani hawasubiri mvua kulima bali hilima pindi tu wakimaliza kuvuna,ambapo ni baada ya kupatiwa elimu na wataalam mbali mbali kutoka Korea na wataalamu wa kituo cha utafiti cha seliani.

Aidha aliwataka wakulima wenzake kuacha kupanda zao moja badala yake wapande mazao mchanganyiko kwa kuzingatia yenye rutuba sambamba na kujiegemeza katika kilimo cha umwagiliaji kwani ni ukombozi tosha kiuchumi.

Kwa upande wake  mwenyekiti wa mkutano huo Stephen Dominick Lyimo ambaye pia ni afisa mtafiti kilimo mkuu wa kituo cha Selian alisema kuwa lengo la mkutano huo ni kuwasaidia wakulima wa kilimo cha mseto kuinuka kiuchumi kutokana na shughuli za kilimo ikiwemo kuwapatia pembejeo za kilimo.

Alisema kuwa mradi huo wa kuwasaidia wakulima unalenga pia wakujulisha wakulima masoko ya bidhaa zao kwa bei inayolipa jasho lake ambapo wamelenga kuwanufaisha wakulima 30,000 katika wilaya 5 za Meru, Siha, Kilosa, Moshi na Arusha na sasa wameshanufaisha wakulima 7,000.

Alisema kuwa awali kabla ya kuanza kwa mradi huo walifanya utafiti na kugundua kuwa wakulima wengi hulima bila kutumia mbolea hata za ruzuku,hawaandai mashamba kabla ya kulima, wakivuna hawajui masoko ya kupeleka matokeo yake hulanguliwa hivyo kwa sasa wameanza kushughulikia hayo kwa kuwaelimisha wakulima.


0 comments:

Post a Comment